News

Posted On:: Mar, 30 2021
News Images

Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo leo wamekubaliana kushirikiana katika kusukuma mageuzi katika sekta ya filamu nchini.


Kamati hiyomachi 29, 2021 ilikuwa ikisikiliza maelezo ya Wizara ya Habari kuhusu maboresho katika Kanuni za Sheria ya Filamu na maoni yaliyotolewa na wadau ili kuiimarisha tasnia hiyo.

"Sekta ya filamu ni kubwa duniani na hapa nchini nikiwaangalia viongozi wa sasa wa wizara naona kabisa wadau wakitoa ushirikiano na kuwa tayari kwa mageuzi tutafika mbali," alisema Ridhiwani Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambayo leo aliongoza kikao hicho.

"Sisi kwa sasa tumekubaliana kuongeza spidi katika utendaji wetu katika kuhakikisha tunaleta mageuzi katika sekta hizi," alisema Waziri Innocent Bashungwa.

Katika mageuzi ambayo yameshaanza kutekelezwa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amesema tayari Serikali imeanzisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni.

"Na Mfuko huu utakaokuwa mkombozi kwa wadau wetu wa sanaa wakiwemo wale wa filamu umeshatengewa bajeti katika mwaka ujao wa fedha. Kazi kwao wadau wetu, wajibu wao ni kuyaunga mkono mageuzi haya ili twende pamoja," alisema Dkt. Abbasi.