Habari

Imewekwa:: Mar, 31 2020
News Images

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka watangazaji na watumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kudumisha weledi na kujituma ili wengine wapate kuiga mambo mazuri kutoka kwao.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa studio mpya ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) inayojengwa katika eneo la ofisi hizo zilizopo Mikocheni. Aidha Dkt. Mwakyembe alizindua Programu Tumizi (App) ya Safari Channel, pamoja na mfumo mpya wa upashanaji habari unaofahamika kama TBC Aridhio ambapo neno Aridhio linamaanisha taarifa au habari.

“Tuna deni kubwa la kuhakikisha tunadumisha weledi na kujituma hivyo kuendelea kuwa kiongozi wa habari hapa nchini, lazima TBC kiwe ni chombo cha rejea,wakitangaza wengine mtu awe na shauku ya kujua TBC imesema nini kwanza”,amesema Dkt.Mwakyembe.

Kwa upande wake, katibu Mkuu wa Wizara ya habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amewapongezawafanyakazi wa shirika hilo kwa hatua hiyo kubwa ya kuleta mapinduzi na ubunifu katika tasnia ya habari katika chaneli hiyo ya ya Tanzania inayotegemewa na taifa.

Mabadiliko haya makubwa ya upashanaji habari ndani ya TBC yanakuja baada ya miaka 13, ambapo safari hii ilianza mwaka 2007. Ujenzi wa jengo hilo la kisasa umeanza Februari, 2020 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.38/- na unatarajiwa kukamilika Agosti 2020, ambapo hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 20.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo mpya wa upashanaji habari Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayoub Rioba amesema kuwa kutokana na mahitaji ya sasa ya dunia ya sayansi na teknolojia imelazimika mifumo ya zamani ya upashanaji habari kupinduliwa na kuja na namna mpya za upashanaji habari. Aidha Dkt. Ayoub Rioba ameishukuru Wizara kwa namna ambavyo imekuwa bega kwa bega katika kuunga mkono mafanikio ya Shirika hilo.