Habari

Imewekwa:: Nov, 15 2018
News Images

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe amewaahidi viongozi wa Veta kufikisha vilio vya changamoto zao kwa viongozi husika.

Mheshimiwa Mwakyembe ameyasema hayo leo jijijni Dodoma alipokuwa akizindua Tamasha la Michezo na Maonesho ya vyuo vya ufundi Kanda ya Kati Dodoma,mara baada ya viongozi hao kusoma risala yao kuhusu tamasha lao ambalo litadumu kwa wiki nzima lengo likiwa ni kujenga umoja na kuboresha mahusiano kwa vyuo vya ufundi pamoja na kuweka mikakati ya kutoa elimu bora yenye kusaidia taifa kufika malengo ya uchumi wa Kati na nchi ya viwanda.

“Kwanza ninawapongeza sana kwa kutambua umuhimu wa michezo katika kuwajenga vijana wenye ujuzi ambao wanaelewa thamani ya michezo kwani michezo ni afya na michezo ni ajira kwa hakika jambo hili mlilolifanya ni jambo zuri na pia natoa rai kwenu wanamichezo wote mnaoshiriki michezo hii kucheza kwa amani ,“alisema Mhe.Dkt.Mwakyembe.

Akiendelea kuzungumza katika uzinduzi wa tamasha hilo Mhe.Mwakyembe alisisitiza kuwa katika mashindano hayo asingependa kusikia kuwepo kwa wachezaji mamluki ambao siyo wanamichezo kutoka katika vyuo husika vilivyoshiriki tamasha hilo.

Pamoja na hayo nae Naibu Waziri Ofisi ya Mkuu Ajira Kazi Vijana na Walemavu Mhe.Anthony Mavunde alieleza mipango mbalimbali serikali iliyojiwekea ya kushirikiana na VETA kwa ajili ya kuhakikisha inawasaidia vijana kupata mafunzo ya ufundi ambayo yatawawezesha kujiajiri na kufanikisha adhima ya nchi yetu kufikia uchumi wakati na nchi ya Viwanda.

“Kupitia umoja huu wa vyuo vya ufundi kwa kanda ya kati waliyouanzisha nitajitahidi kuwasimamia na kuhakikisha wanaanzisha kiwanda chao wenyewe cha mfano ,“Mhe.Mavunde.

Aidha,nae Kaimu Mkuu wa Chuo Veta Kanda ya Kati Bw.Ramadhan Mataka alieleza kuwa VETA kama wasimamizi wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufundi nchini hivi karibuni uongozi wa Kanda ya Kati imevifungia vyuo ishirini vilivyokuwa havina viwango vya kutoa mafunzo kukuzingatia sheria na utaratibu wa hadhi ya vyuo vya ufundi.

“Kupitia Umoja wa Vyuo vya Ufundi tunataka tuunde mkakati madhubuti wa kuboresha kozi zetu na kuhakikisha tunatoa mafunzo yenye ubora ambayo yatatusaidia wote kutembea katika njia moja kwa manufaa ya taifa letu na uchumi wa nchi yetu,”Bw.Mataka.

Sambamba na hayo Bw.Mataka alitoa rai kwa vyuo vyote vya ufundi vilivyopo Kanda ya Kati ambavyo havijasajiliwa vijisajili haraka ili kurasimisha shughuli zao,”Bw.Mataka

Halikadhalika nae Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyuo vya Ufundi Dodoma, Bw.Jeremia Philip alieleza kuwa umoja huo unamalengo mbalimbali ikiwemo kuboresha masomo ya mafunzo ya ufundi na kuwaongezea vijana ujasiri wa kujiajiri mara baada ya kufuzu masomo yao.

Pamoja na hayo Bw.Jeremia alieleza kuwa umoja huo umeanzisha mpango wa kurudisha darasani vijana ambao hawakupata elimu waliyochini ya miaka kumi na tano wa kuwapeleka darasani na kuwapatia mafunzo ya ufundi kwa lengo la kuwasaidia kuweza kujikwamua kiuchumi.