News

Posted On:: May, 31 2021
News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, anatarajiwa kufungua Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA) Juni 8, 2021 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Akitoa taarifa kwa umma leo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amesema mashindano ya UMITASHUMTA yafanyika Juni 6-19, 2021 ambapo UMISSETA yataanza Juni 19 hadi Julai 3, 2021.

"Jumla ya washiriki wapatao 3,600 kutoka Mikoa yote Tanzania Bara wanatarajiwa kushiriki katika michezo ya UMITASHUMTA na washiriki 3,800 kutoka Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki katika michezo ya UMISSETA," amesema Prof. Shemdoe.

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameitaja michezo itakayohusika kuwa mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, mpira wa mikono, mpira wa meza, riadha jumuishi, kwaya na ngoma. Aidha, mchezo wa mpira wa kikapu utahusisha shule za Sekondari kwa wavulana na wasichana.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. James Mdoe, amesema michezo inajenga afya, ubunifu, upendo, hali ya kujiamini na umoja wa kitaifa.

"Serikali imekwisha elekeza kuendelea na uimarishaji wa ufundishaji wa michezo shuleni sambamba na kuendeleza na kuimarisha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA katika ngazi zote ikiwemo hii ya Taifa," ameeleza.

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema viongozi wa mashirikisho na vyama vya michezo ili wajionee vipaji na kwamba mashindano hayo yatarushwa mubashara kupitia TV mbalimbali nchini.

"Tutaendelea kuboresha michezo hii ili iwe kitovu cha kuandaa, kukuza na kuuza vipaji vya vijana wetu," amedokeza Dkt. Abbasi.

Aidha, amesema zaidi ya wachezaji 26 hivi sasa katika ligi kuu na ligi ya daraja la kwanza wametokana na mashindano hayo huku ikitoa takriban asilimia 95 ya wachezaji wa timu za soka za vijana.

Amesema pia mashindano hayo ambayo ufunguzi wake utapewa burudani na wasanii mbalimbali maarufu wa muziki wa kizazi kipya, kwa sasa yameboreshwa ili kuhama kutoka tukio la kawaida la michezo shuleno hadi kuwa tukio kubwa la kimichezo la kitaifa na kuwa kitovu cha mawakala wa vipaji kusaka nyota wa michezo mbalimbali.