Habari

Imewekwa:: Sep, 16 2019
News Images

Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe awapongeza wazee na viongozi wa kimila wa kabila la kimasai kwa kuendeleza na kuhifadhi mila na desturi.

Hayo ameyasema leo Ngaramtoni, Jijini Arusha wakati wa kufunga mafunzo ya kimila kwa vijana wa kimasai na kueleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kumjenga kijana kuwa mtu mwenye maadili na kuheshimika kwa jamii yake.

“Mafunzo haya mliyoyapata kutoka kwa viongozi wenu na Wazee wa kimila yanawajenga kuwa rai wema na wenye maadili katika kujenga taifa letu ” Dkt. Mwakyembe

Aidha aliongeza kwa kueleza kuwa Wizara inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Wazee wa Kimasai kwa kuhakikisha mila na desturi ya mtanzania inatunzwa na kuendelezwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Pia Dkt. Mwakyembe ameahidi kushirikiana kwa karibuna Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi katika kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za mila yanahifadhiwa vizuri bila kuingiliwa na watu.

Vilevile aliwapongeza viongozi wa Jeshi la Tanzania kwa kuruhusu maeneo ya kijeshi ambayo ni ya kihistoriakuendelea kutumika ajili ya masuala ya kimila na kuzitaka taasi nyingine ambazo zina maeneo hayo kuiga mfano huo .

Naye Mwenyekiti wa Viongozi wa Ukoo wa Wamasai Bw. Isack Lekisongo ameiomba serikali kulinda, kuhifadhi na kuendeleza mila na desturi za jamii mbalimbali za kitanzania ili kupunguza madhara yanayoletwa na utandawazi.

“Ni muhimu kwa serikali yetu kutilia mkazo suala la kuhifadhi na kuendeleza mila za jamii mbalimbali zilizopo nchini ili kuwa na taifa lenye kuheshimu na kudumisha tamaduni zake” Bw. Isack Lekisongo

Anazidi kueleza kuwa kupitia mafunzo hayo yanayotolewa kwa vijana yanawasaidia kujitambua,kuheshimu wakubwa na wadogo pamoja na kuachana na tabia zisizofaa ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya.

Shughuli hizo za kimila za kimasai zilifunguliwa tarehe 6 Julai 2019 kwa vijana kutoka katika sehemu mbalimbali za Tanzania pamoja na nchi jirani ya Kenya ambao walipewa mafunzo kwa muda wa siku 100 na kuhitimishwa tarehe 15 Septemba 2019 huku Dkt. Mwakyembe Waziri mwenye dhamanaya utamaduni akiwa ndiye mgeni rasmi.