News

Posted On:: May, 10 2021
News Images

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ametoa maelekezo mahususi kwa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuwataka kusitisha utekelezaji wa Kanuni ya 25 ya mwaka 2018, inayotaka kazi zote za Sanaa kukaguliwa na Baraza hilo kabla ya kusambazwa.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo Mei 08, 2021 katika kikao chake na Viongozi wa Vyama na Mashirikisho ya Muziki na Filamu nchini kilicholenga kuzungumzia Kanuni ya 25 ya BASATA inayohusu uhakiki wa kazi za Sanaa kabla ya kuingia sokoni au kusambazwa.

Mhe. Bashungwa amesisitiza kuwa maelekezo hayo ya kusitishwa kwa matumizi ya Kanuni hiyo ni kwa upande wa Muziki pekee ila kwa upande wa Filamu itaendelea kutumika kama kawaida.

"Nawaelekeza BASATA kuharakisha mchakato wa kurekebisha Kanuni hiyo kwa kuwashirikisha wadau wao wa vyama na mashirikisho ili kuweza kupata Kanuni mpya isiyodumaza Tasnia ya Muziki lakini izingatie maadili ya Taifa" alisisitiza Mhe.Bashungwa.

Aidha Waziri huyo ameelekeza BASATA kushirikiana na wadau kuandaa mwongozo utakao kuwa ukitoa dira njema ya uendeshaji na ukuzaji wa tasnia ya Muziki.

Mhe. Bashungwa pia amewatoa hofu Wasanii kuhusu suala la ugawaji wa Mirabaha kwa kuelezea kuwa Serikali imeandaa mifumo ya kidijitali ambayo itarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo na kuongeza gawio.

"COSOTA imekuwa na changamoto ya ukusanyaji wa mirabaha kutokana na uhaba wa watumishi hivyo kwa kupitia mfumo mpya wa kidijitali utakao anzishwa hivi karibuni utarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo, Serikali inataka kutoa gawio la pesa nyingi kwa wasanii na siyo fedha kidogo hivyo tunawaomba mvumilie kidogo kuanzia mwaka mpya wa fedha mambo yatakuwa mazuri,"Mhe.Bashungwa.

Naye mmoja wa wasanii hao Soggy Doggy alimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa maamuzi aliyoyafanya na kumpongeza ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na wasanii wenzake katika Muziki ili kukuza na kuiendeleza tasnia hiyo.