News

Posted On:: Feb, 21 2021
News Images

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abassi pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusuph Singowafike jijini Arusha kukutana na uongozi wa mkoa pamoja na wadau wa riadha ili kuhakikisha mchezo huo unarudi katika uhai wake kama ilivyokuwa awali.

Waziri Bashungwa amesema hayo leo jijini Arusha baada ya kumaliza kufanya mazoezi yaliyoshirikisha Jogging Club ya jijini humo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo hatua inayosaidia kuimarisha afya za wananchi.

“Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tunaleta uhai na ufanisi mkubwa kwenye riadha, tujipange upya tuinue mchezo wa riadha Tanzania, si soka peke yake ama mchezo wa baiskeli, watu wafanye mazoezi kuimarisha afya na kujiepusha na magonjwa ya kuambukiza, mlipuko na yasiyoambukiza” alisema Waziri Bashungwa.

Aidha, ametoa wito kwa Wakuu wa Wilaya wote nchini kupitia halmashauri zao kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi na kuhamasisha waendelee kuratibu jogging katika maeneo yao ili kuwasaidia wananchi kujihami kiafya ili kulinda afya zao hatua inayosaidia kupunguza gharama za matibabu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenan Kihongosi akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Arusha Iddi Hassan Kimanta amesema mkoa huo pamoja na wilaya zake zipo mstari wa mbele katika kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha mchezo wa riadha na michezo mingine.

Naye mdau wa riadha mkoa wa Arusha Amani Ngoka ametoa ombi kwa Mhe Waziri ambapo amesema wakimbiaji wa mbio fupi nchini pamoja na wanariadha ambao wanaulemavu wamesahaulika na ameomba mbio hizo zipewe nafasi ili washiriki wake waweze kukua katika medani hiyo hatua itakayosaidia kufikia viwango vya kimataifa na kuliwakilisha taifa katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha, baada ya kumaliza mazoezi ya viungo ili kuweka utimamu wa mwili, wanamichezo hao waliungana na Watanzania wote kuliombea taifa hasa katika kipindi hiki ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaka kuliombea taifa na kuliweka chini ya ulinzi wa Mungu huku wakichukua tahadhari za kiafya kulingana na mwongozo uliotolewa na Wizara yenye dhamana na afya

Mazoezi ya kukimbia yalihusisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya Kenan Kihongosi, Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo, viongiozi mbalimbali pamoja na wanchi wakiongozwa na kikundi cha wana jogging Arusha ambapo mazoezi hayo yalikuwa ya umbali wa Zaidi ya kilometa tisa kuanzia ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Arusha kupitia barabara ya Sanawari, Philips kuelekea Impala na kurudi ofisi ya Mkuu wa Mkoa.