News

Posted On:: Oct, 13 2021
News Images

Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Mkichezo Dkt. Hassan Abbasi amesema Wasanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka Tanzania wanatarajia kupamba mashindano ya Urembo na Mitindo kwa Viziwi Barani Afrika yatakayofanyika kesho Ijumaa, Oktoba Mosi, 2021, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julias Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam ili kuongeza hamasa ya shindano hili la kihistoria.

Akizungumza kwenye mkutano na Vyombo vya Habari leo Septemba, 30 jijini Dar es Salaam na baadaye katika kikao cha kuwasalimia washiriki hai, Dkt. Abbasi amesema kutokana na umuhimu na upekee wa shindano hili Wizara imewachukua baadhi ya wasanii wa kizazi kipya ambao wamekuwa wakipiga nyimbo kwa mfumo wa kiasili na mahadhi ya Tanzania ili kutambulisha utamaduni wa taifa hili nje ya Tanzania na hatimaye kufungua soko la utalii duniani.

Amewataja baadhi ya wasanii ambao watatumbuiza katika shindano hilo kuwa ni pamoja na Sholo Mwamba, Wanne Star, Saraphina na Z Anto aliyepata kuimba wimbo maarufu wa “Binti Kiziwi.” Wakati Dkt Abbasi akiwataja wasanii hao na kueleza kisa cha wimbo wa Binti Kiziwi washiriki hai waliripuka kwa shangwe wakionesha kufurahja burudani huku wengi wakisema wanaijua Tanzania kama kitovu cha burudani hasa muziki.

“Ndugu zangu tunashukuru kupata fursa hii adhimu ya kuratibu mashindano ya Afika ya Urembo na Mitindo kwa viziwi, kama Taifa tunakwenda kutumia shindano hili kimkakati kutangaza utalii wetu na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini ili kuwavutia wageni kutoka kwenye mataifa mbalimbali duniani." Amefafanua Dkt. Abbasi

Amesema baada ya kufanya shindano hili Wizara imeratibu washiriki wote kutembelea baadhi ya vivutio na kufanya utalii wa kiutamaduni katika maeneo ya Dar es Salaam na Bagamoyo.

Shindano hili limeratibiwa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na Kituo cha Sanaa Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA).

Jumla ya washiriki takribani 60 kutoka nchi 13 Barani Afrika wameshawasili nchini tayari kwa mpambano huo wa kukata na shoka, nchi hizo ni pamoja na wenyeji Tanzania, Siera Leon, Uganda, Kenya, Botswana, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Senegal, Sudani Kusini na Zimbabwe. Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji wa shindano hilo.