Habari

Imewekwa:: Jan, 22 2020
News Images

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe amesisitiza kuwa itakapofika Desemba mwaka 2021 ndio mwisho wa waandishi wa habari wasiokua na elimu kuanzia ngazi ya stashahada kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya habari ya Mwaka 2016.

Waziri Mwakyembe ametoa kauli hiyo jana Mkoani Singida alipokuwa anazungumza na wadau wa tasnia ya habari ambapo amewataka waandishi hao kutambua kuwa kuanzia mwaka 2022 wale ambao hawatakua na vigezo kulingana na Sheria ya Huduma za Habari hawatakua na nafasi wala sifa ya kuitwa Waandishi wa Habari.

“Uandishi wa habari ni taaluma kama taaluma nyingine na sio kimbilio la wale ambao wamefeli katika masomo au waliokosa kazi ya kufanya,hivyo naomba mtambue kuwa mwaka 2021 ndio mwisho wa waandishi wasiokua na elimu ya uandishi wa habari kuanzia ngazi ya stashahada”amesema Mhe.Mwakyembe

Aidha Dkt.Mwakyembe amesema kuwa Ibara ya 18 d ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa kila mwananchi ana haki ya kupata taarifa sahihi hivyo ni jukumu la wanahabari kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa ambazo ni sahihi kutoka kwa watu sahihi na kuzifikisha kwa walengwa kwa usahihi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Mlagiri ameongeza kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo wanahabari wasitumike kuchafua watu,kuandika habari za uongo pamoja na kuepuka kupewa rushwa na watu wanaotaka watumie kalamu zao kuwatafutia kura na badala yake waandike habari za ukweli ambazo zitalinda amani na usalama wa nchi yetu.

“Tumeni kalamu zenu vizuri ili msije kuhatarisha amani ya nchi yetu na pia jiepusheni na kuandika habari kwa kutegemea kupewa pesa na wale wanaowapa habari ili msije mkaingia katika mikono ya Sheria” alisema Eng.Mlagiri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo Bw.Rodney Thadeus amewataka waandishi wa habari kuhakikisha kuwa wanakuwa na kitambulisho cha mwanahabari popote wanapokuwa wanatimiza majukumu yao kwani ndio utambulisho wa tasnia hiyo huku akieleza kuwa vitambulisho vya wanahabri hao kwa mwaka huu tayari vinapatikana katika ofisi yake.

Awali Mhe.Waziri Mwakyembe alifanya ziara ya kukagua mitambo ya usikivu wa redio ya Shirika la Utangazaji TBC iliyopo katika eneo la Mikumbi mkoani hapo ambapo ameeleza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha usikivu wa redio ya Shirika hilo nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dkt.Ayoub Ryoba amesema kuwa mitambo miwili ya Khts 2 kwa kila mmoja imeshawasili nchini tayari kwa kufungwa ili kuongeza usikivu katika maeneo mengi nchini ambapo kwa sasa usikivu umefikia asilimia zaidi ya 70.

“Usikivu wa Shirika la Utangazaji TBC kwa mwaka 2016 ulikua asilimia 54,mwaka 2019 asilimia 67 na mwaka huu tunategemea kufikia asilimia zaidi ya 70 lengo ni kufikia watu wengi zaidi”.alisema Dkt.Ryoba.

Hata hivyo katika ziara hiyo Waziri Mwakyembe amepata nafasi ya kupata historia fupi ya wanawake wawili ambao ni Litti Hema pamoja na litti Kidanka waliopigania uhuru wa kabila la wanyaturu uliofanywa na Mwalimu Alfred Ringi ambapo imeleeza ushiriki wa kila mmoja katika kukomboa kabila hilo kwa kutumia mvua na nyuki ambapo Mhe.Waziri amemuagiza mwalimu huyo kuendelea kutafuta undani wa historia hiyo ili Serikali iweze kuihifadhi.