News

Posted On:: Dec, 03 2020
News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi amesema kuwa Serikali itafanya Tamasha la Serengeti Music and Art Festival Desemba 26, 2020 litakalofanyika katika uwanja wa uhuru.

Dkt. Abbasi ametoa kauli hiyo Leo Desemba 02, 2020 Jijini Dar es Salaam, katika mkutano na wasanii wa tasnia ya filamu ambapo alisisitiza kuwa siku hiyo itakuwa ni maalum kwa ajili ya kusherekea Sanaa za Tanzania.

Akizungumza katika mkutano huo wenye lengo la kujadili mambo ambayo wanatasnia ya filamu wanahitaji Serikali kufanya ili kusaidia tasnia hiyo kukua na kuendelea sanaa, Dkt. Abbasi alieleza kuwa Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ambao utasaidia kutoa mikopo rahisi kwa wasanii na kutoa elimu, upo tayari na hivi karibuni unatarajia kuanza kazi.

"Serikali imesikia kilio chenu cha muda mrefu kuhusu changamoto mbalimbali za kupata maeneo ya kufanyia kazi na inampango wa kujenga eneo ambalo litakuwa na vitu vingi ikiwemo sehemu ya kufanya matamasha ya Sanaa “Arts Arena” na tayari ameshapatikana mtaalamu anayechora ramani ya mradi huo na tunatarajia kujenga kituo cha kisasa,"alisema Dkt.Abbasi.

Pamoja na hayo kufuatia malalamiko ya baadhi Wasanii wa Filamu wanawake juu ya unyanyasaji wa kingono kutoka kwa Waandaji wa Filamu wanaume Dkt.Abbasi ameilekeza Bodi ya Filamu Tanzania kufungua dawati la jinsia kusimamia hilo.

Naye Msanii wa Sanaa za Maonesho ya Jukwaani Bw. Ian Mwaisunga aliomba Serikali kupunguza ada za tozo kwani wamekuwa wakilazimika kufanya matamasha ya bure bila kuweka kiingilio kutokana na gharama za tozo pale uwanapoweka kiingilio.

Halikadhalika Katibu Mkuu Baraza la Sanaa la Taifa Godfrey Muingereza aliahidi kulifanyia kazi suala la kupunguza tozo hizo katika Kanuni zinazofanyiwa marekebisho hivi sasa.