Habari

Imewekwa:: Jun, 25 2020
News Images

Serikali imewataka wasanii wa Sanaa ya choraji (Tingatinga) kujisajili katika Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili waweze kunufaika na kazi zao na kuepuka kuibiwa na kuzulumiwa haki zao kama ilivyo hivi sasa.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam Wakati Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alipowatembelea wasanii hao kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali wanazokutana wasanii hao katika kazi zao.

“Wassanii tumieni fursa hii ya mabadiliko ya sheria kwa kuhakikisha mnasajili kazi zenu COSOTA ili muweze kunufaika na kazi zenuvilevile kuepuka kuibiwa na kudhulumiwa haki zenu,” alisema Naibu Waziri Shonza.

Aidha Naibu Waziri Shonza amesema kuwa Wizara inaendelea na mchakato wa kuihamisha COSOTA toka Wizara ya Viwandana Biashara kuja Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo hatua iliyofikiwa ni kukamilisha andiko la pamoja kwa ajili ya kuwasilisha katika mamlaka za uamuzi.

“Tunafanya hivyo ili kuhakikisha vyombo vinavyoshughulikia haki, maslahi na upatikanaji wa huduma kwa wasanii vinakuwa chini ya mwamvuli mmoja ili kuwaondolea usumbufu, gharama na hata upotevu wa stahilli zao,” alisema Naibu Waziri Shonza.

Vilevile Naibu Waziri amewashauri wasanii hao wafanye kazi zao kwa weledi kwa kuzingatia hali ya mabadiliko ya teknolojia kwa kutumia njia za mitandao kuuza kazi zao na kulifikia soko la nje hata katika mazingira magumu kama ya ugonjwa wa COVID 19 (Corona).

Nae Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Ushirika cha Tingatinga Bi. Zena Salum ameiomba serikali ameiomba serikali kuwatafutia viwanja kwa ajili ya kufanyia shughuli zao kwani kwa sasa wanachangamoto ya maeneo ya kufanyia kazi zao.

“Tunaiomba serikali itupatie maeneo ya kufanyia kazi zetu kwani kuna haja ya kupata miundombinu ya kisasa kwani kwa asilimia tisini wateja wetu ni kutoka nchi za nje,” alisema Bi. Zena Salum.

Sanaa ya uchoraji imeendelea kupewa kipaumbele na serikali ikiwa ni pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 1999 ili iweze kuendana na mazingira ya sasa na kumnufaisha msanii.