Habari

Imewekwa:: Dec, 31 2019
News Images

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Ally Possi ameutaka uongozi Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kubadilika kiutendaji na kuwa walezi wa wasanii badala ya kuwa polisi.

Dkt.Possi ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za Baraza kwa lengo la kupata taarifa za utekelezaji wa majukumu yao na kufuatilia utekelezaji wa mpango mkakati wa majukumu ya taasisi hiyo.

Akiendelea kuzungumza katika ziara hiyo Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa katika dunia ya leo Sanaa ndiyo tasnia yenye fursa nyingi za kiuchumi hivyo ni vyema taasisi hiyo ikasimama wasanii na kuwajibika katika kuwalea ili kuondoa dhana iliyopo kwa sasa ya kuonekana inafanya kazi kama polisi badala ya kusimama katika jukumu lake halali la kusimamia sanaa na kuibua vipaji vya wasanii.

“Shirikianeni na wasanii katika mazingira mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu juu ya taratibu ya utekelezaji wa shughuli za sanaa ili hata pale wanapokosea na nyinyi mnapowachukulia hatua waweze kuona mchango wenu badala ya kuwaacha wajiongoze bila kuona jitihada zenu katika kuwapatia fursa halafu wanapokosea mnakimbilia kuwafungia hii inawaharibia taswira yenu sababu hawaoni mchango wenu katika kuendeleza kazi zao,”alisema Dkt. Possi.

Pamoja na hayo Dkt.Possi alitoa maelekezo kwa uongozi huo wa Basata kuhakikisha unakamilisha Kanuni za Sheria ya Basata wizarani pamoja na Mpango mkakati wa taasisi hiyo mwishoni mwa mwezi Februaria 2020, ili kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za baraza unakwenda sambamba na mahitaji ya wadau wao ambayo wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kanuni hizo.

Aidha, nae Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bibi.Joyce Fisoo aliwasihii viongozi wa Baraza kuharakisha mchakato wa kurasimisha shughuli za sanaa kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia zaidi katika kuongeza ukusanyaji wa mapato kwani wanauwanja mpana wa kukusanya fedha kupitia sanaa.

“Angalieni namna ya kujipanga na kuwa na programu ya kuibua vibaji kwa wasanii pia tafuteni fursa za kurudisha matamasha yatakayowasaidia wasanii na kuona mchango wenu,mfano tamasha la Kilimanjaro Music Award jipangeni kuwa na kitu kama hichi tena,”alisema Bibi.Fisoo.

Nae Mhasibu Mkuu wa BASATA Bw.Onesmo Kayanda aliyemuwakilisha Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa katika risala yake alitoa ombi kwa wizara kuwaombea fedha hazina kiasi cha bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ukumbi wa sanaa za maonesho.

Mbali na hayo mmoja wa wafanyakazi wa Baraza la Sanaa la Taifa Bibi.Vivian Shalua ambaye ni Afisa Sanaa alitoa neno la shukrani kwa niaba ya wafanyakazi wenzake na kushukuru uongozi wa wizara kwa kutembelea ofisi hiyo na kuwaeleza ukweli juu ya kutoridhishwa utendaji wao kwakuwa changamoto kubwa ni hali ya kutozingatia uendeshaji wa majukumu kwa kuzingatia fani na kuwemo kwa migogoro baina yao.

Halikadhalika Pamoja na hayo Dkt. Possi aliwataka viongozi na watumishi wa taasisi hiyo kuacha migogoro kwani hiyo ndiyo inayokwamisha utekelezaji wa shughuli za Baraza na kufanya kushindwa kuwatekelezea majukumu yao ya kuwahudumia wadau vyema.