Habari

Imewekwa:: Nov, 26 2019
News Images

Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa vyombo vya kiroho na viongozi wake katika kuliombea taifa lidumishe amani na upendo ambavyo ni msingi katika maendeleo.

Akizungumza katika kwenye maadhimishio ya Jubilei ya fedha ya miaka 25 ya upadre wa Mhashamu Askofu Liberatus Sangu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema mafanikio makubwa tunayoyapata kiuchumi kama taifa yatakosa uhai (sustainability) bila baraka za Mwenyezi Mungu.

Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye alialikws kuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo Dkt. Mwakyembe aliwapongeza Askofu Liberatus Sangu na mapadre wote watimiza miaka 25 ya utume wao wa upadre kwa kazi nzuri iliyotukuka na yenye tija kwa taifa.

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo katoliki la Shinyanga Liberatus Sangu amemshukuru Mungu kwa kuijalia nchi yetu kuwa na viongozi wanyoiongoza kwa majitoleo yao na kusisitiza kuwa “Ukiona vyaelea ujue vimeundwa”.

“Tunaipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayofanya, mwenye kubeza kwa miaka mine hii, anapaswa kuchunguzwa akili yake, kama ana akili nzuri basi ana wivu. Leo tupo hapa kwa sababu tuna uhuru wa kuabudu” Askofu Liberatus Sangu.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi alitoa salamu za mkoa huo na kusema mkoa wake una amani ya kutosha na kuwasisitiza wananchi tujitokeze Novemba 24 mwaka huu kuchagua viongozi wa Serikali za mitaa ambao watafaa na kuwaletea maendeleo na kuwahimiza wananchi watumie vizuri muda wao kwa kazi ya kilimo kwa kuwa msimu wa mvua umeshaanza katika mkoa huo.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Maaskofu Wakuu wa Mjimbo Makuu, Maaskofu wa Majimbo Katoliki kutoka mikoa yote nchini, mapadre, watawa wa kiume na wakike, viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na vyama vya siasa na maelfu ya wakazi wa Shinyanga na mikoa jirani yakiongozwa na kauli mbiu ya utumishi wa uaskofu wa Mhashamu Sangu “Tunda la Roho ni Upendo.”