Habari

Imewekwa:: Mar, 20 2020
News Images

Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza amemsisitiza

mwandaaji wa filamu ya Dalton kuhakikisha anaisambaza filamu hiyo kila mahali ili kuwapa fursa

watoto kujifunza.

Mhe.Shonza ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza alipokuwa akizindua filamu hiyo

yenye kutoa elimu kwa watoto namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana

nazo katika jamii.

"Filamu hii niya kipekee sababu imebeba maudhui mazuri ambayo yanatoa elimu kwa watoto na

ni vyema ikaonyeshwa katika vipindi vya watoto katika televisheni badala ya watoto kuangalia

katuni tu,"alisema Mhe.Shonza.

Akiendelea kuzungumza Naibu Waziri huyo aliwasisitiza wazazi kuwa makini na katuni

ambazo watoto wao wanaangalia kwani baadhi ya katuni hizo zinamaudhui ambayo siyo

mazuri na zinachangia mmomonyoko wa maadili.

Pamoja na hayo naye mtayarishaji wa filamu hiyo Bw. Cherrif Daudi alimwahidi

Naibu Waziri huyo kuwa atahakikisha katika kuisambaza filamu hiyo mikoa yote nchini.

"Niliamua kuandaa filamu hii sababu niliona familia nyingi zimeshindwa kutenga muda

wa kuongea na watoto kuhusu kusimamia ndoto zao na namna ya kukabiliana na

changamoto wanazokutana nazo katika jamii,pamoja na kuwa na utii,uwajibikaji na

kutokata tamaa,"alisema Bw. Daudi.

Aidha,nae Bw.Daudi aliendelea kusisitiza kuwa ni imani yake filamu hii itakuwa

mkombozi kwa watoto na vijana katika kutoa elimu kuhusu mmomonyoko wa maadili.

Pamoja na hayo nae Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana Bw.Jonas Maduhu alimpongeza

mheshimiwa Naibu Waziri Shonza kwa namna wizara yake anavyofanya kazi kwa bidii ya

kusimamia wasanii na pamoja na kuwasapoti katika kazi zao.

Halikadhalika nae mmoja ya wanafunzi waliyohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa

filamu ya Dalton kutoka Shule ya Kingdom Heritage School Joan Mwalukasa wa Darasa la tano

alieleza kufurahishwa na filamu hiyo na namna inavyotoa elimu ya maadili kwa watoto na

kufundisha kuhusu heshima kwa wakubwa.

Katika kuhitimisha Mhe.Shonza aliwasisitiza wasanii wa mwanza kujisajili BASATA ilikuendesha

shughuli zao katika mfumo rasmi,pamoja na kupendana na kuhakikisha wanazalisha kazi zenye

ubora pamoja na muandaaji wa filamu ya Dalton kujipanga kuwa na programu ya kuibua vipaji

vya watoto.