News

Posted On:: May, 03 2021
News Images

Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekulamesema kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) hayajawahi kubadili Katiba zao kwa lengo lakuwalinda viongozi walioko madarakani, bali suala hilo lazima lizingatie mabadiliko ya Kikatiba na lazima likidhi vigezo vinavyosimamiwa na Msajili wa Vilabu vya Micheo Nchini.

Mhe. Gekul amesema hayo Mei 03, 2021 Bungeni Jijini Dodoma, alipokua akijibu Swali la Mheshimiwa Ravia Idarus Faina wa Jimbo la Makunduchi aliyeuliza Je,Kwanini Vyama vya Michezo ikiwemo TFF na TOC vimekua vikibadili Katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi walipo madarakani na kudhibiti Watanzania wengine wasigombee katika vyama hivyo.

Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Gekul ameeleza kuwa Vyama vya Michezo Tanzania vimesajiliwa kwa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa na 12 ya Mwaka 1967 na marekebisho yake Na.6 ya mwaka 1971 na pia namba 3 ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni za Msajili za mwaka 1999.

“Pamoja na mahitaji ya kubadili Katiba za Vyama kujitokeza na kufanyika, Katiba hizo haziwezi kuanza kufanya kazi mpaka zisajiliwe upya na Msajili wa Vyama ambaye hupitia upya kuona kama mabadiliko hayo yanaendana na matakwa ya Sera,Sheria na Kanuni zinazosimamia Michezo na Sheria nyingine za nchi”amesisitiza Mhe.Gekul.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Sofia Mwakagenda aliuliza swali ya nyongeza kuhusu Kwanini viongozi wa TOC wanagombea kwa vipindi vitatu hali inayonyima uhuru wa watu wengine kugombea, ambapo Mhe. Naibu Waziri Gekul ameeleza kuwa Kamati hiyo imeendelea kufanya marekibisho ya vipengele mbalimbali kwenye Katiba yao ili kutoa uhuru kwa wengine kugombea.

“Novemba mwaka 2020 Msajili aliweza kupitisha kanuni kuwa mtu akigombea nafasi ya Rais anatakiwa awe amehudumu kwa sehemu tatu ya miaka minne, na baada ya hapo asirudie kugombea nafasi hiyo anatakiwa kugombea nafasi za juu kwenye Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) au nafasi nyingine” amesema Mhe. Gekul.

Vilevile Naibu Waziri Gekul ameongeza kuwa iwapo Msajili atabaini kuwa Suala ambalo limeingizwa katika Katiba halina maslahi kwa Chama na Taifa ikiwemo masuala ya Utawala Bora, Msajili amepewa Mamalaka kisheria ya kukataa usajili huo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili za mwaka 1999 kifungu 11(3) (a) na (b).

Hata hivyo Mhe. Gekul alitumia nafasi hiyo kuwatakia heri Wanahabari nchini na Duniani katika kuadhimisha siku ya leo ya Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.