News

Posted On:: Nov, 15 2021
News Images

Wadau wa michezo wamehimizwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la sekta hiyo iendelee kuwa chanzo adhimu cha ajira kwa vijana nchini.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amesema Sekta za Wizara hiyo ni miongoni sekta kongwe zilizoanzishwa nchini tangu Tanzania Bara ilipopata uhuru miaka 60 iliyopita hadi sasa.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari Novemba 13, 2021 jijini Dodoma kuhusu katika mkutano na waandishi hao kuhusu miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Mhe. Gekul amebainisha kuwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imebeba miongoni mwa sekta kongwe na za mwanzo kuundwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, licha ya kuwa sekta hizo zimekuwa zikiwekwa katika Wizara mbalimbali.

“Watanzania hatujafikia hatua ya kujitoa akili kiasi hicho, ni lazima kusimamia utamaduni na maendeleo ya utamaduni wetu na taifa, bado tupo imara” amesema Naibu Waziri Gekul.

Akimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere Naibu Waziri Gekul amesema “Utamaduni ni kiini ama roho ya taifa lolote, taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho.”

Tangu Tanzania Bara ilipopata Uhuru mwaka 1961, Wizara hiyo imekuwa kinara wa kusimamia na kuhakikisha Taifa linaendelea kuenzi Utamaduni imara wa Mtanzania, kuwa na kazi bora za Sanaa na taifa lenye umahiri mkubwa katika michezo ambapo mwaka 1962 Serikali ya kwanza iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana hatua inayodhihirisha kuwa ni sekta nyeti na muhimu katika kusimamia masuala ya utamaduni wa nchi.

“Ninatumia nafasi hii kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuona umuhimu wa sekta hizo kwenye Serikali yake ya Awamu ya Sita na kuzipatia kipaumbele. Ni ukweli usiopingika kuwa tumeshuhudia mafanikio makubwa sana katika kipindi hiki kifupi, amesema Mhe. Gekul.

Akitolea mfano, Mhe. Gekul amesema katika sekta ya michezo miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na eneo la soka la wanawake ambako kumekuwa na makombe mengi ya kimataifa kuliko wakati wowote, kufufua mashindano ya michezo ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na sekondari (UMISSETA) ambayo yanazalisha vipaji vya wanamichezo; na kuanzisha tamasha kubwa la michezo kwa wanawake la Tanzanite lililotoa hamasa kubwa kwa wanawake kufanya vizuri kwenye michezo.

Ameongeza kuwa Tanzania tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika kwa sasa Tanzania Bara na kufikia mafanikio lukuki katika sekta Sekta ya Michezo nchini ikiwemo ambapo jumla ya Medali 16 katika michezo mikubwa kabisa duniani ambayo ni ya Olympic mbili, Jumuiya ya Madola saba, na Michezo ya Bara la Afrika saba, na kwamba timu zetu zimeshiriki katika michezo hii mikubwa bila kukosa tangu tupate uhuru wetu.

Katika kukuza ajira kwa vijana nchini, hadi sasa nchi yetu imefanikiwa kuwa na wachezaji wakulipwa katika nchi mbalimbali tangu uhuru wa patio wachezaji 54 wakulipwa katika nchi mbalimbali ambapo 28 ni wachezaji wa mpira wa miguu, 16 mpira wa kikapu, wachezaji wanne wanacheza mpira wa wavu, wawili Kabbadi, wawili Netiboli, mmoja kuogelea na mchezaji mmoja mchezo wa Roliball.

Katika eneo la miundombinu ya michezo, Naibu huyo amesema Tanzania imepiga hatua kubwa ambapo viwanja vya michezo mbalimbali vimeboreshwa na kujengwa na Serikali pamoja na wadau wa Michezo ikiwa ni pamoja.

Amevitaja viwanja hivyo kuwa ni pamoja na Uwanja wa Benjamini Mkapa uliogharimu Shilingi Bilioni 56.4, Kituo cha Michezo cha JK Park cha jijini Dar es Slaam, Majaliwa Stadium kilichopo Ruangwa mkoani Lindi, Azam Complex, Black Rhino cha mjini Karatu, Ngarenaro Complex Arusha na viwanja vya Golf ambavyo vipo mikoa mbalimbali.

Viwanja vingine ni pamoja na Viwanja vya Uhuru, Nyamagana na Kaitaba ambavyo tayari vimewekewa nyasi bandia, kuboreshwa kwa uwanja wa Ndani wa Taifa pamoja na kuwekwa taa kwa viwanja vya Jamhuri Dodoma na Majaliwa Stadium.

Hatua hiyo imepelekea Serikali kutenga fedha katika mwaka wa fedha wa wa 2021–2022 kiasi cha Shilingi Bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Michezo katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita na Dodoma.

Mkakati mwingine wa Serikali ni kuanzishwa na kuongezeka kwa vituo vya kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana katika michezo ambapo mpaka sasa kuna vituo 136 vilivyo sajiliwa hapa nchini.

Vituo hivyo ni pamoja na Alliance Academy, Azam Soccer Academy, Fountain Gate Academy na katika kuunga mkono juhudi za Serikali miradi ya maenndeleo wa FIFA, TFF inaendelea na ukamilishaji wa vituo vikubwa viwili katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam, eneo la Kigamboni.

Hivyo, katika mwaka wa fedha 2021–2022 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha kisasa katika Chuo cha Michezo Malya kwa lengo la ukuzaji na uendelezaji wa vipaji vya michezo mbalimbali pamoja na kuteua shule 56 ambapo katika kila mkoa ili kuwa na shule maalumu zisizopungua mbili kwa ajili ya kulea na kuendeleza vipaji vya michezo kwa wanafunzi.

Hakika mafanikio hiyo ni mwanzo mpya unaotokana na maono yenye tija na uongozi thabiti wa Wizara chini ya Jemedari Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuru ya Muungano wa Tanzania ambayo yamejengwa kwenye dhima ya Taifa ya kukuza Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa lengo la kuleta maendeleo ya jamii kiuchumi kwa kuongozwa na kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Sita “Kazi Iendelee”.