News

Posted On:: Apr, 16 2021
News Images

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameelekeza Mamlaka ya Mawasiliano - TCRA kukaa mara moja na Viongozi wa Vyombo vya habari vya Taasisi za Dini nchini (TAREMA - Tanzania Religious Media Association) kutatua changamoto zinazokabili Taasisi hizo.

Mhe. Waziri ametoa maagizo hayo katika kikao kilichofanyika ofisi za wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) 15 April 2021 jijini Dar es Salaam kati ya Taasisi hizo na Mmamlaka hiyo ambapo ameiagiza TCRA kuwa na utaratibu wa kila mwaka kuwa na mkutano utakaowakutanisha na wadau wao ili maamuzi yatakayofanyika yatumike katika mabadiliko ya sera pamoja na uendeshwaji wa vyombo vya habari.

“Nawapongeza viongozi wa vyombo vya habari vya taasisi za dini nchini kwa kazi kubwa mnayoifanya ambayo imekuwa msaada kwa Taifa kwa kutoa mafundisho ambayo yamekuwa yakikitolewa kupitia TV, Radio na Magazeti ambayo mmekuwa mkiyasimamia” alisema Mhe.Waziri Bashungwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAREMA, Mtume Venon Vanandez ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutatuachangamoto zinazokabili Vyombo vya Habari pamoja na kupokea ushauri unaotoa, huku akitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa Serikali na Wananchi kupitia Mhe. Bashungwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na kumpongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha amani ya nchi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa TAREMA, Sheikh Hassan A. Hassan kwa niaba ya viongozi wote ni ameiomba Serikali kupitia TCRA ishughulikie suala la kurudisha Leseni za vyombo vya habari visivyo vya kibiashara (Non - Commercial broadcasting Licenses) pamoja na Kurudishwa kwa daraja la Reginal License kama ilivyokuwa awali, ambapo Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inafanyia kazi suala hilo.