Habari

Imewekwa:: Aug, 19 2020
News Images

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kwa ujenzi wa uwanja wa Majaliwa Stadium ambao unajengwa kwa kuzingatia viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Dkt. Mwakyembe ametoa pongezi hizo Agosti 12, 2020 alipotembelea uwanja huo ambapo amesema kuwa eneo la kuchezea (pitch) lina nyasi bora ambazo zina viwango vinavyohitajika katika viwanja vya soka duniani.

“Uwanja huu utakapokamilika utakuwa ni uwanja wa kisasa, kwasababu ujenzi wake unazingatia viwango vya kimataifa ikiwemo vyumba bora vya wachezaji kubadilishia nguo, maduka ya kuuza jezi mbalimbali, majukwaa ya hadhi tofauti, hivyo naipongeza sana Halmshauri ya Ruangwa kwa uwekezaji huu”alisema, Dkt. Mwakyembe.

Aidha, Dkt.Mwakyembe ameishauri halmashauri hiyo kufikiria kuweka nyasi bandia katika uwanja huo kwakua nyasi hizo zinatumia gharama nafuu katika utunzaji na zinasaidia shughuli mbalimbali kufanyika bila kuharibika tofauti na nyasi halisi.

Vilevile Waziri Mwakyembe ameipongeza halmashauri hiyo kwa kuilea vizuri timu ya Namungo FC ambayo imefanya vizuri katika ligi kuu na mashindano ya Kombe la shirikisho hatua iliyoifanya timu hiyo kufuzu kuiwakilisha nchi katika Kombe la shirikisho barani Afrika.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa Halmshauri hiyo Bw.Fundikira Masamalo amesema kuwa uwanja huo utakua na majukwaa mbalimbali ikiwemo jukwaa kuu na jukwaa la mashabiki takriban 1,200.

Uwanja huo unatarajiwa kuwa na viwango vinavyofanana na Uwanja wa Benjamin Mkapa wa jijini Dar es Salaam na utatumika katika ligi mbalimbali na michezo mingine.