Habari

Imewekwa:: Sep, 03 2020
News Images

SHIRIKA la Utangazaji Tanzania (TBC) ni chombo cha utangazaji cha Umma chenye lengo la kuhabarisha na kuelimisha wananchi kuhusu utekelezaji wa Sera, mipango, maagizo na maelekezo ya Serikali yenye lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Kutokana na umuhimu huo, Shirika hili limehakikisha kuwa mikoa yote ambayo ilikuwa na changamoto ya usikivu kwenye chaneli zake za redio zaTBC Taifa na TBC FM katika mikoa ya Njombe, Lindi, Mtwara,Tanga, Kilimanjaro pamoja na Visiwa vya Pemba na Unguja zimetatuliwa.

Maboresho ya usikivu yaliyofanywa ni dhamira thabiti ya Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kuwa wananchi wa wilaya zote 161 nchini wanapata matangazo ndani ya kipindi cha miaka mitano. Katika kipindi cha miaka mitano usikivu wa TBC umeongezeka kutoka asilimia 54 mwaka 2015 hadi 86 mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha, mabadiliko hayo yanatokana na mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kuwa kila mtanzania popote alipo anapata matangazo yanayorushwa na redio za TBC.

“TBC imepata mafanikio haya kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia bajeti ya Miradi ya Maendeleo iliyopanda kutoka Shilingi bilioni moja kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/17, hadi kufikia shilingi bilioni tatu kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18”.

Dkt. Ryoba amefafanua kuwa Mwaka wa fedha 2018/19, 2019/20 na 2020/2021, fedha za kupanua usikivu wa TBC ziliongezeka kwa kiasi cha shilingi bilioni tano kwa kila mwaka wa fedha kwa miaka yote mitatu. Ongezeko hilo limesaidia kununua mitambo na vitendea kazi mbalimbali.

Hivi Karibuni katika ziara ya kukagua mitambo ya TBC nchini, Mhandisi wa Shirika hilo Bibi. Upendo Mbelle ameeleza kuwa shirika hilo linaendelea kuimarisha usikivu katika maeneo yote nchini kwa kununua na kusimika mitambo mipya na kuboresha mitambo mingine ambayo inahitaji kurekebishwa katika baadhi ya maeneo.

“Kupitia fedha za Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, Shirika litafunga mitambo katika baadhi ya maeneo ikiwemo maeneo ya Ludewa na Makete Mkoani Njombe ambapo tayari maeneo ya kusimika mitambo hiyo yamepatikana, Hivyo kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2020/2021 usikivu utakuwa umeimarika zaidi” alisema Bibi Upendo.

Kutokana na uimarishaji huo TBC imekusudia kuhakikisha kuwa vyombo vyake vyote vya habari vinaboreshwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi, huku ikiendelea kutekeleza lengo lake la kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha sehemu kubwa ya watanzania nchini kote.