News

Posted On:: Aug, 30 2019
News Images

Katibu Mkuu Bibi Susan Mlawi amewata wadau wa Sekta ya Sanaa na Utamaduni kuchangamkia fursa ya kujisajili kushiriki Tamasha la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) kwani siku zimebaki chache kuelekea kufungwa kwa dirisha la usajili.

Bibi.Mlawi ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma alipofanya kikao na Kamati ya Maandalizi kupata mrejesho wa hatua mbalimbali za maandalizi zilipofikia kutoka kwa kamati ndogondogo zinazoandaa tamasha hilo.

‘’Tumebakiza siku chache sana takribani wiki tatu kufikia siku za tamasha hivyo ni vyema tukajipanga vyema siku za hivi karibuni kwa kufunga dirisha hili la usajili ili tuweze kupanga namna ya kuratibu shughuli hizi kwa kuzingatia idadi ya watu kwani tukichelewa italeta changamoto katika ufanisi wa maandalizi haya,’’alisema Bibi.Mlawi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha Kitaifa Bibi.Joyce Fissoo alisema mpaka sasa zaidi ya washiriki 900 wamekwisha jisajili kwa ajili ya kushiriki tamasha hili kutoka nchini na suala hili la usajili tunatarajia kulifunga baada ya wiki moja kuanzia sasa.

‘’Tunashukuru wadau wa Sekta ya Utamaduni na Sanaa nchini walivyoweza kujitokeza kujisajili kwa hii ni fursa kubwa katika jukwaa letu la afrika mashariki na fursa hii siyo ya kukosa kwani ita chukua miaka mingi sana mpaka tamasha hili litakapo rudi tena nchini, ‘’ alisema Bibi.Fissoo.

Tamasha hili litafanyika jijini Dar es Salaam Uwanja wa Taifa na litakuwa na Zaidi ya shughuli kumi na moja ikiwemo Maonesho ya Vyakula vya Asili,Michezo ya Jadi na Maonesho ya Kazi za Sanaa na Ugunduzi na lengo la Tamasha hili ni kuboresha mahusiano ya kikanda.