Habari

Imewekwa:: Sep, 12 2019
News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi.Susan Mlawi amewapongeza vijana wanne waliofanya vizuri katika mafunzo ya uaandaaji wa Filamu yalioandaliwa na Kampuni ya Multichoice yaliyofanyika nchini Kenya ambapo amewataka kutumia taaluma waliyopata kutengeneza filamu bora zenye maudhui ya kuitangaza nchi yetu na kuleta ushindani katika soko.

Katibu Mkuu Bibi. Susan ameyasema hayo leo ofisini kwake Jijini Dodoma baada ya kutembelewa na vijana hao ambao amewataka kufika katika Bodi ya Filamu Tanzania kuwasilisha uelewa waliopata na kushauri namna ambavyo Bodi hiyo inaweza kuwatumia katika tasnia hiyo.

“Nawapongeza sana kwa kufanya vizuri katika mafunzo mliopewa,naamini mtayatumia vizuri katika kukuza vipaji vyenu na kusaidia mawazo kwa wengine ambao hawajapata nafasi hii,Lakini pia mtatumia ujuzi na taaluma mliyopata katika kuleta mapinduzi ya utengenezaji wa filamu hapa nchini”alisema Bibi Susan.

Naye Meneja wa masuala ya Biashara wa Kampuni ya Multichoice Bw.Jonson Mshana amesema kuwa Kampuni hiyo imeanzisha dawati la kusaka vipaji vya uandaaji wa kazi za filamu (Multichoice talent Factory Academy) kwa Bara la Afrika ili vijana wenye uwezo na vipaji kupata fursa ya kuongezewa maarifa pamoja na kutafuta ajira kwa njia rahisi.

Bw.Jonson ameongeza kuwa Kampuni hiyo kila mwaka inatafuta vijana wanne ambao wanapatikana kwa kuomba nafasi hiyo na hatimaye kufanyiwa usaili na kujiunga na wenzao kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika ikiwemo Kenya,Ethiopia, Uganda na Nigeria.

Naye Kijana Jamal Mohamed Kishuli ambaye amejifunza “Art Designer” amesema kuwa vijana wanapaswa kujiamini katika kila wanachokifanya na kutokata tamaa lakini pia zinapotokea fursa za kuonyesha uwezo wao basi wasisite kujitokeza ili kupata nafasi ya kujitangaza kupitia vipaji walivyonayo.

Vijana hao walikua katika mafunzo ya Uandishi wa Mswada (Script Writer), Uandaaji (producer) Uongozaji (Directing) na Art Desgner ambayo wamejifunza kwa mwaka mmoja katika Chuo Kikuu cha Kenyata nchini Kenya.