Habari

Imewekwa:: Jul, 18 2020
News Images

Wazee wa jamii za kitanzania wasisitizwakurithisha mambo ya utamaduni kwa watoto na vijana ili tamaduni hizo ziweze kuendelea kwa vizazi vijavyo.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu alipokuwa katika ziara kutoa Elimu ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Urithi wa Utamaduni alipotembelea kikundi cha Utamaduni cha Nyati Mchoya, kilichopo katika Kijiji cha Nzali, Kata ya Chilonwa, Dodoma.

“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuwarithisha watoto na vijana shughuli za utamaduni hii inasaidia mambo haya kuendelea hata kwa vizazi vijavyo na msipofanya hivi mnahatarisha asili ya utamaduni wenu kupotea,”alisema Dkt.Temu.

Akiendeleza kuzungumza katika ziara hiyo Dkt. Temu alisema kuwa serikali inataka kupanua wigo wa utalii na kuifanya sekta ya Utamaduni kuwa ya utalii hivyo nijukumu la kila mtanzania kulinda na kuhifadhi utamaduni wake kwani nchi hii inautajiri mkubwa katika sekta hiyo ambao unaweza kukuza uchumi wa mwananchi kwa urahisi zaidi kutoka na namna ya uendeshaji wake.

Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo aliendelea kutoa wito kwa watanzania kuwa wanajitokeza kwenda kuangalia burudaniza utamaduni kama wanavyojitokeza kwenda kutazama mpira, na kusema serikali inatarajia kuanzisha matamasha mbalimbali ya utamaduni kwa lengo la kukuza na kutangaza utamaduni wa mtanzania.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Maadili na Urithi wa Taifa Bw.Boniface Kadili alipongeza uongozi wa vikundi vilivyotoa burudaniya ngoma kwa namna walivyonesha sanaa yao kwa kuzingatia kuzingatia uchezaji wa asili ambao hauna kuiga watu wa nje, zana za jadi walizotumia pamoja na uvaaji wa maleba.

Aidha, naye Kiongozi wa Kikundi cha Nyati Mchoya Bw. John Mchoya alitoa ombi kwa wizara la kusaidia baadhi ya vikundi visivyo na uwezo wa kujisajili BASATA pamoja na kusaidia vikundi hivyo vidogo kupata fursa za kushiriki shughuli mbalimbali ikiwemo matamasha na shughuli za serikali.

Halikadhalika nae mmoja wa kikundi cha Msamaria Bibi. Rhoda Petro alishukuru uongozi wa wizara kwa kuwatembelea na kuwa kutoa elimu ya namna ya kuhifadhi utamaduni wao na kuwaomba kurudi tena wakati mwingine.