Habari

Imewekwa:: Sep, 16 2019
News Images

Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa ni muhimu kwa lugha ya Kiswahili kuwa na kanuni ambazo zitasaidia katika kufanikisha mawasiliano kwa jamii ili kuleta maendeleo chanya.

Hayo aliyasema leo Jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa kanuniza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) lengo ikiwa ni kuwazesha kusimamia matumizi ya lugha.

“Ni muhimu kwa kila lugha kuwa na kanunina sifa kubwa ya lugha ya Kiswahili ni unyumbulifu, hivyo ninaamini kupitia kanuni hizi tutakuwa na usimamizi mzuri wa matumizi ya lugha hii” Dkt. Mwakyembe

Aidha aliongeza kwa kueleza kuwa lazima kanuni hizo ziwe nyumbulifu na rafiki ili kuweza kuzifanyia marekebisho endapo kutakuwa na mapungufu yoyote wakati wa utekelezaji wake.

Pia aliwapongeza wataalamu wote kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali walioweza kufanikisha upatikanaji wa kanuni hizo na kuwataka kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kukuza, na kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Dkt. Selemani Sewange alilezea kuwa kuzinduliwa kwa kanuni hizo ni mojawapo ya mafanikio makubwa kwa lugha ya Kiswahili.

“Leo tunaweka historia nzuri katika nchi yetu kwa hatua hii muhimu ya kufanikisha uzinduzi wa kanuni za lugha ya Kiswahili ambazo pia zinatupa fursa ya kuwa na marekebisho kwa kadri zitakavyokuwa zinatekelezwa” Dkt. Sewange.

Historia inaeleza kuwa Baraza la Kiswahili la Taifa liliundwa na sheria ya bunge Na. 27 ya mwaka 1967 kwa shabaha ya kukuza, kuimarisha na kuendeleza Kiswahilinchini na baadaye kufanyiwa marekebisho mwaka 1983 kwa sheriaya Bunge Na. 7 ikiwa imepewa uwezo wa kufuatilia na kusaidia ukuzaji wa Kiswahili nje ya nchi na baadayesheria hiyo ilifanyiwa marekebisho ya mwisho mwaka 2016.