Habari

Imewekwa:: May, 15 2020
News Images

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amewataka Wanasheria wa Wizara yake kuingia makubaliano ya kisheria na Kampuni ya Ujenzi ya ‘Tanzania Building Works LTD’ inayotaka kuyatumia majengo ya Wizara yajulikanayo kama magofu ya BMT kuhifadhia vifaa vyao.

Ameyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kilichohusu kurejea kwa ligi ambapo alimtaka Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Mohamed Iqbal Noray kuwaleta wataalam wao ili waje kuyakagua majengo hayo kama yatafaa kwa matumizi kabla ya kufanya makubaliano nao.

“Majengo haya yanaonekana kuwa hayafai kutumiwa kutokana na kujengwa katika kiwango kisichoridhisha, sasa kabla ya kufanya makubaliano na Wizara yangu leteni wataalam wenu waje kukagua kwanza kama yanafaa kwa matumizi” alisema Dkt. Abbasi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Ujenzi, Mohamed Iqbal Noray alisema kuwa kampuni yake iko tayari kulifanyia ukarabati jengo moja watakalolitumia na watakapokamilisha kazi yao watalikabidhi kwa Wizara lakini pia watasaidia kuyabomoa majengo mengine.

Awali Katibu Mkuu Dkt. Abbasi alifanya kikao na viongozi wa michezo kuhusu kurejea kwa ligi ambacho kilichowahusisha Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo, Watendaji wakuu wa Baraza la Michezo la Taifa akiwemo Mwenyekiti Leodiger Tenga na Kaimu Katibu Mtendaji Neema Msitha, Katibu Mkuu TFF Alfred Kidau, Mkurugenzi wa Bodi ya ligi Almasi Kasongo ambao alijadiliana hatima ya kurejea kwa lig nchini.