Wasifu

DKT. HASSAN ABBASI
KATIBU MKUU
DKT. HASSAN ABBASI

Dkt Hassan Abbasi alizaliwa wilayani Korogwe, Tanga mwaka 1978 na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Hale kati ya mwaka 1988 na 1994. Alimaliza akiwa mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri mkoani humo na kujiunga na Sekondari ya wanafunzi wenye vipaji maalum ya Tabora Wavulana (Tabora School) mwaka 1995 kwa masomo ya sekondari.

Kati ya mwaka 1997 na 1998 alihamia katika Sekondari ya Azania, Dar es Salaam ambapo alimaliza kidato cha nne na kati ya mwaka 1999-2001 alijiunga na Shule ya Sekondari Lindi kwa masomo ya kidato cha tano na sita.

Kati ya mwaka 2002 na 2006 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alichukua shahada ya kwanza ya sheria (LL.B). Akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu pia aliajiriwa kama mwandashi wa habari wa kujitegemea katika kampuni ya Business Times na baadaye kushika nafasi mbalimbali kuanzia mwandishi mwandamizi, mhariri msaidizi hadi mhariri mkuu katika magazeti ya Majira na Kulikoni.

Mwaka 2005 akiwa bado mwanafunzi, alichaguliwa kuwa Mhariri Mkuu wa Jarida liitwalo “Nyerere Law Journal” linalochapishwa na Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kati ya mwaka 2007 na 2008 alihudhuria masomo ya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi ikiwemo makao makuu ya Reuters, London, Uingereza na Chuo Kikuu cha Maine nchini Marekani.

Mwaka 2010 aliajiriwa Serikalini akiwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) tawi la Tanzania, programu iliyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Nje kabla ya mwaka 2014 kuwa Meneja Mawasiliano katika Ofisi ya Rais, Kitengo cha Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Agosti 5, 2016. Pamoja na taaluma ya sheria ambako ana hadhi ya Wakili wa Mahakama Kuu tangu mwaka 2011, Dkt. Abbasi pia ana diploma ya uzamili katika usimamizi wa mahusiano ya kimataifa (PGD-MFR) kutoka Chuo cha Diplomasia cha Msumbiji na Tanzania, Kurasini, shahada ya uzamili katika mawasiliano kwa umma (MA Mass. Comm., SAUT) na shahada ya uzamivu katika mawasiliano kwa umma (Ph.D Mass. Comm., SAUT).