Faida za Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika

FAIDA ZITAKAZOPATIKANA KUTOKANA NA PROGRAMU YA URITHI WA UKOMBOZI WA BARA LA AFRIKA KUTEKELEZWA NCHINI TANZANIA

Utekelezaji wa Programu hii unazo faida nyingi zikiwemo zifuatazo:

a) Tanzania kuwa ngome na kitovu cha kuhifadhi na kuendeleza urithi hasa urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika;

b) Kukuza utalii wa Kiutamaduni na utalii wa Kiukombozi ambao ni aina mpya ya utalii. Hii itasadia kupata fedha za kigeni na kuinua kipato cha nchi;

c) Kuhifadhiwa vema kwa ushahidi wa namna nchi yetu ilivyosaidia kwa hali na mali nchi za Kusini mwa Afrika na Bara zima la Afrika kutasaidia kutanabahishwa kwa mchango wa Tanzania katika kuongoza mapambano ya kutafuta uhuru wa Bara la Afrika;

d) Wasanii watahamasishwa na kujengewa uwezo wa kuandaa kazi za kiubunifu ili kuenzi Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika na kupitia kazi hizo wasanii watainua kipato chao;

e) Taifa litafaidika kutokana na wasanii wa ndani na nje ya nchi kutumia mandhari ya maeneo ya Urithi wa Ukombozi katika kuandaa kazi mbalimbali za Sanaa kama vile Filamu na muziki;

f) Kuwajengea uwezo wataalam wa Taasisi zinazojihusisha na masuala ya urithi hususani katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali za urithi wa utamaduni;

g) Kuboreshwa kwa mitaala ya elimu hususani Mtaala wa somo la Historia ili masuala ya urithi wa utamaduni na urithi wa ukombozi yaweze kufundishwa katika ngazi zote za elimu nchini, Hii itawezesha kizazi kilichopo na kijacho kuelewa namna wazee wetu walivyolikomboa Taifa letu dhidi ya ukoloni na namna Nchi yetu ilivyosaidia kwa hali na mali Nchi zingine za Afrika hadi Bara zima lilivyokombolewa;

h) Kutekelezwa kimadhubuti kwa Mikataba ya Kimataifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ambayo Nchi yetu imesharidhia tangu mwaka 2011. Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa UNESCO wa mwaka 2003 unaohusu Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni usioshikika, Mkatabwa wa UNESCO wa mwaka 2005 unaohusu uhifadhi na uendelezaji wa uanuwai wa kujieleza kiutamaduni;

i) Kukuza ajira miongoni mwa Wataalam na wadau mbalimbali wa masuala ya utamaduni na urithi;

j) Kukuza uelewa wa wataalam wa urithi katika kuhifadhi masuala ya urithi kwa njia ya kidijiti (TEHAMA);

k) Kuwawezesha Wataalamu wa uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni kubadilishana uzoefu na mbinu mbalimbali za uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni na Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.

l) Kuwa na wigo mpana wa kushirikiana na Nchi mbalimbali za Afrika katika kuyatambua na kuyaorodhesha maeneo ya Urithi wa Ukombozi yaliyopo hapa nchini katika orodha ya Urithi wa Dunia; Nomination of the African Liberation Heritage Sites in the World Heritage Lists.