ZINGATIENI MAADILI NA UWAJIBIKAJI KATIKA KUTEKELEZA MAJUKIMU YENU: NAPE


Imewekwa 08th December, 2016

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amewataka watendaji na watumishi wa Wizara yake kuzingatia maadili na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ameyasema hayo wakati akifungua Baraza la wafanyakazi la Wizara yake na kusisitiza kwa watendaji kuwasimamia watumishi walio chini yao kuzingatia maadili na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao katika kutoa huduma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa kuwepo kwa ushirikiano kati ya uongozi na watumishi utasaidia kufanikisha masuala mbalimbali ya maendeleo ya Wizara, Taasisi zake na watumishi katika kuleta maendeleo ya Wizara katika kutimiza wajibu wao.

“Nawataka watumishi wazingatie maadili katika kutekeleza wajibu wao na naamini kwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano tutarudisha maadili ya Utumishi wa Umma na bado taratibu zinaendelea kusimamiwa ipasavyo”asisitiza Mhe Nnauye.

Mhe. Nnauye amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ana mpango wa dhati wa kurujesha maadili katika Utumishi wa Umma na kuhakikisha heshima yake inarudi.

Alieleza kuwa endapo kuna mtumishi yoyote atakayeshindwa kusimamia suala zima la maadili anapoteza utumishi wake.

“ Wananchi ndiyo tunaowatumikia na ndiyo wanaotufanya tuwepo hapa tulipo wanahitaji huduma bora. Kama hatutazingatia suala la maadili ni hakika hatutaweza kuwatumikia vema” alieleza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara hiyo , Prof Elisante Ole Gabriel ameahidi kutekeleza agizo hilo kwa kuhakikisha watumishi wanazingatia maadili na suala hili linafanyika kwa vitendo zaidi na sio maneno ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli za kurudisha maadili katika Utumishi wa Umma.

“Mhe. Waziri nakuahidi mimi pamoja na watendaji wenzangu tutalisimamia suala hili na kulitekeleza kwa vitendo ili turudishe heshima ya utumishi wa Umma kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kurudisha uaminifu kwa wananchi”alisema Prof Gabriel.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi Magreth Mtaka amesema kuwa ni jambo muhimu kwa watumishi kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao katiKa eneo la kazi.

“Niwashauri watumishi wenzangu tuzingatie maadili ya Utumishi wa Umma ili turudishe heshima ya utumishi wa umma na tutoe huduma iliyo bora kwa wananchi” alisema Bibi Magreth.