Vyombo vya Habari vya Serikali vimetakiwa kufuata Maadili ya Uandishi wa Habari


Imewekwa 24th October, 2017

Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amevitaka vyombo vya habari vya serikali kufuata maadali na miiko ya uandishi wa habari kwa kuzingatia weledi ili umma eweze kupata habari zilizokidhi vigezo vya uandishi wa habari.

Rai hiyo ameitoa jana jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) pamoja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na kuzungumza na watendaji wa taasisi hizo.

“Vyombo vya habari vya serikali viwe mfano bora kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa watanzania wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kwani vyombo hivi ni moja kati ya mhimili mkubwa wa nchi na kama vitatumika vibaya madhara yake ni makubwa sana” amesema Mhe. Shonza

Aidha Mhe. Shonza amesema kuwa Serikali inathamini na kutambua mchango unaotolewa na vyombo vya habari vikiwemo vyombo vya serikali TBC katika kufikisha taarifa za ukweli na uhakika katika jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Dkt. Ayob Rioba amemhakikishia Mhe. Shonza kuwa TBC itaendelea kuzingatia weledi na maadili katika kuhabarisha umma huku ikiendelea kubuni vipindi mbalimbali vitakavovutia jamii kuangalia televisheni hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa TSN imeendelea kuhakikisha kuwa taifa linahabarishwa kwa hakika kwa kutumia nyenzo mbalimbali na uzoefu tangu ilipoanzishwa miaka 88 iliyopita hivyo kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu

“kwa sasa TSN ni zaidi ya magazeti, imejikita zaidi kuwa kampuni inayotoa huduma za habari kwa kutumia nyenzo mbalimbali za kiteknolojia ili kuweza kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na taknolojia” amesema Dkt. Yonazi.