Tumieni Mashirikisho ya Sanaa na Filamu kuinua sanaa yetu kitaifa na kimataifa:- Mwakyembe


Imewekwa 13th February, 2018

Viongozi mashirikisho ya Sanaa na Filamu nchini wametakiwa kuongeza juhudi katika kusimamia uboreshaji wa kazi za sanaa na filamu ili ziweze kuthaminiwa na kukidhi matakwa ya walaji kwa kuwafanya kupenda vya kwetu

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harison Mwakyembe alipokutana na viongozi hao kujadili masuala mbalimbali yaliyofanywa na kuelekezwa na Serikali leo Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mwakyembe amesema kuwa kama Mashirikisho ya Sanaa na Filamu nchini yatazingatia uboreshaji wa kazi za sanaa zetu itapelekea kuua soko la kazi za sanaa kutoka nje ya nchi hivyo kuinua kipato cha wasanii na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Sanaa Bibi. Leah Kihimbi ameyataka mashirikisho ya Sanaa na Filamu nchini kuwa na meno ya kusimamia vyama vilivyopo nchini ya mashirikisho yao na kuhakikisha kuwa shughuli zote za sanaa zinazofanywa na vyama vyao zinapita kwenye mashirikisho husika ili ziweze kufuata taratibu za mashirikisho hayo.

Aidha Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo ameyataka mashirikisho ya sanaa kufuata sheria, kanuni na taratibu za kutafsiri kazi za filamu za nje kwa kuwa na kibali cha mmiliki wa filamu husika pamoja na mswada wa filamu wa lugha mama ya filamu husika inayoambatana na mswada wa filamu wa lugha ya kiswahili