TANZANIA TUTOENI KIMASOMASO KATIKA MICHUANO YA JUMUIYA YA MADOLA APRIL 2018; MHE. MAMA SAMIA.


Imewekwa 10th April, 2017

Timu za michezo nchini zinazotarajia kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola mwakani nchini Australia zimeombwa kuanza maandalizi mapema ili ziweze kuitoa Tanzania kimasomaso katika mashindano hayo kwa kushinda medali nyingi na kuliweka jina la Tanzania katika ramani ya ulimwengu wa michezo.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan jana Jijini Dar es Salaam wakati akipokea kifimbo cha Malkia wa Uingereza kuashiria maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya Madola April 2018 nchini Australia.

Mhe. Samia amesema kuwa ujumbe wa Tanzania ulioambatana na kifimbo cha Malkia wa Uingereza umezingatia urithi na ufahari wa maliasili zilizopo Tanzania unaosema “tukomeshe ujangili wa wanyama pori tuwaache waishi”.

“Tunapoteza urithi na ufahari wetu, ni wajibu wa kila mtanzania kushirikiana na serikali katika kuwalinda wanyama pori na rasilimali zetu katika kuendeleza urithi wa nchi yetu” alisema Mhe Samia.

Aidha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa mashujaa walioiletea Tanzania medali za mashindano ya Jumuiya ya Madola wawe chachu na dira kwa wanamichezo watakaoshiriki mashindano hayo mwaka 2018.

Mhe. Dkt. Mwakyembe amesema kuwa ni wajibu wa Serikali katika kuwatunza na kuwalea wanamichezo ili waweze kushindana na kupata ushindi utakaoletea nchi heshima ambapo ameahidi kuwa Wizara itashirikiana na vyama vya michezo kuandaa wachezaji mapema ili kupata wachezaji wenye uwezo na sifa katika mashindano hayo.

“Ni vyema vyama vya michezo kutoa ushirikiano katika kutafuta wachezaji ambao wana uwezo kwakuwa wao ndio wanawafundisha na kuwajua uwezo wao katika michezo” Alisema Mhe. Mwakyembe.

Kifimbo cha Malkia wa Uingereza kinakimbizwa katika nchi 71 za Jumuiya ya Madola kabla ya mashindano yanayotarajiwa kufanyika huko Australia April 2018 ambapo Tanzania ni nchi ya 08 kupokea kifimbo hicho kinachohamashisha amani, upendo na mshikamano kuelekea mashindano hayo.