PROF. ELISANTE OLE GABRIEL AWAOMBA WADHAMINI KUJITOKEZA KUDHAMINI MICHEZO YA WANAWAKE.


Imewekwa 10th April, 2017

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel ameomba wadhamini kujitokeza kudhamini michezo ya wanawake ili itambulike na kupata mafanikio hapa nchini.

Kauli hiyo ameitoa leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa anazindua Kongamano la wanawake na Michezo liliondaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambapo amesema kuwa michezo inahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadhamini hivyo ni wajibu kwa wadhamini mbalimbali kuona jitihada zinazooneshwa na wanawake na waziunge mkono.

“Michezo inaleta ni afya lakini pia inaleta umoja na ushirikiano katika kutafuta maendeleo ya jamii nawaomba wadhamini mjitokeze kuunga mkono jitihada hizi za wanawake ili zilete mafanikio,” Alesema Prof Elisante Ole Gabriel.

Aidha Katibu Mkuu huyo amewataka viongozi wa vyama vya michezo vya wanawake kuwa wabunifu katika kutafuta fursa zilizopo katika michezo ili waweze kufanikiwa zaidi pamoja na kusimamia yale waliyoazimia kwa maendeleo ya Michezo yao.

Kwa upande wake Bibi Jenifer Mmasi Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa amesema kuwa kongamano hilo lina lengo la kuwakutanisha wanawake ambao ni wanamichezo kupata ujuzi na namna bora ya kutumia michezo katika jamii zao kama njia ya kutatua changamoto malimbali za maendeleo.

“Ni vizuri kwenu viongozi kutumia fursa hii kujifunza zaidi ili mnapokuwa katika maeneo yenu muwaelimishe wanawake wengine umuhimu wa kushiriki katika michezo,”Alisema Bibi Jenifer.

Kongamano hilo la siku moja linalenga kujadili jinsi wanawake wanavyoweza kufanikiwa kupitia michezo pamoja na changamoto ambazo wanawake wanakutana nazo katika kushiriki michezo na kuzitafutia ufumbuzi.