MHE. ANASTAZIA WAMBURA AAHIDI KUSHIRIKIANA NA WIZARA NYINGINE KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO.


Imewekwa 13th December, 2016

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni imeahidi kuhakikisha kuwa mila na desturi zenye kuchochea ukatili dhidi ya wanawake na watoto zinakwisha kabisa.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Anastazia Wambura wakati akiwasilisha mchango wa Wizara yake katika uzinduzi wa Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa mwaka 2017/18 hadi 2021/22.

“Tutaendelea kushirikiana na Wizara nyingine hasa TAMISEMI kuhakikisha kuwa Maafisa Utamaduni na Sanaa wa kila Halmashauri wanaisaidia jamii kuelewa maana na madhara ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini kupitia kazi za mbalimbali za sanaa na utamaduni” alisema Mhe.Anastazia.

Alizidi kufafanua kuwa Wizara itashirikiana na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini katika kutafuta na kutoa habari kuhusu vitendo vya ukatili vinavyofanywa dhidi ya wanawake na watoto kwa kuelimisha umma kuhusu adhari zake.

Vilevile alisisitiza kuwa kupitia sekta ya Michezo itaanzishwa kampeni maalum ambayo kabla ya mchezo kuanza na wakati wa mapumziko hadhira iliyopo katika tukio hilo inapata elimu kuhusu ubaya na madhara ya ukatili dhidi ya watoto na wanawake.

Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa mwaka 2017/18 hadi 2021/22 umeshirikisha Wizara tisa ikiwemo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ,Mashirika ya Umoja wa Mataifa(UNCEF, UN-WOMEN, UNFPA, WHO na ILO),Wawakilishi kutoka katika Taasisi zisizo za Serikali pamoja na wanawake na watoto huku Serikali ikitenga bajeti ya shilingi Bilioni 267.4 ambapo kwa mwaka 2017/18 imetengwa shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya kutekeleza mapango huo.