Kukabidhi Bendera wachezaji wanaokwenda Mashindano ya Jumuiya ya Madola Australia


Imewekwa 04th April, 2018

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe amewataka wachezaji wanaokwenda katika mashindano ya Jumuiya ya Madola kuhakikisha wanashindana kwa bidii na kurudi na medali.

Mheshimiwa Mwakyembe ametoa msisitizo huo katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya kukabidhi bendera kwa wanamichezo kumi na sita wanaotarajia kuondoka nchini kesho kuelekea nchini Australia katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika katika Mji wa Gold Coast.

“Katika mashindano haya nendeni mkijua mmeiwakilisha nchi na watanzania zaidi ya milioni hamsini wanaimani na nanyi hivyo hakikisheni mnashindana kwa nguvu zote kwa ajili ya kuletea taifa heshima huku mkiangazia kurudi na medali za dhahabu, michezo ni ajira,”alisema Mhe Dkt. Mwakyembe.

Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo Waziri huyo aliendelea kusisitiza kuwa kuanzia mwakani serikali itahakikisha wanamichezo wanaoshiriki mashindano ya kimataifa kuwa wamefanya maandalizi ya kutosha na siyo ya kubababisha ni bora katika mashindano ya kimataifa aende hata mtu mmoja kuliko kwenda kundi la watu asiyokuwa na maandalizi ya kutosha.

Pamoja na hayo nae Kaimu Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa Bi. Neema Msita alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya michezo kuwasilisha mpango kazi wa vyama vyao pamoja na kalenda za kutekelezaji wa shughuli zao kwani kukosekana kwa mambo hayo kumechangia kuwepo na ushiriki mdogo wa vyama vichache katika mashindano haya ya Jumuiya ya Madola kwa mwaka huu ikilingalishwa mashindano yaliyopita.

Kwa upande wa Katibu Kamati ya Olimpiki Tanzania Bw. Filbert Bayi alitoa taarifa kwa Mheshimiwa waziri ya kuwepo na baadhi ya wamichezo wa timu ya taifa ya riadha kutokubali kukaa kambini katika kipindi cha mazoezi ya maandalizi hivyo kutaka vyombo vyenye mamlaka kumchukulia hatua kwa mujibu wa sheria kukomesha tabia kama hizo kwa wachezaji wengine.

Hata hivyo nae Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Bodi ya Utalii Tanzania alieleza kuwa bodi hiyo wametoa udhamini kwa wanamichezo hao kwa kuwapatia tisheti na mashati yatakayo wasaidia kutangaza utalii wa nchi pamoja na jarida lenye kueleza juu ya vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ambalo watahitajika kugawa kwa wenzao watakapofika huko.

Hata hivyo timu zinazoshiriki katika mshindano hayo ni Timu ya Riadha,Timu ya mchezo wa Ngumi,Timu ya kuogelea na Timu ya Mpira wa Tenisi.