Dkt.Mwakyembe Awataka Wadau wa Michezo, Muziki na FilamuMkoani Arusha Kujisajili.


Imewekwa 13th March, 2018

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harisson Mwakyembe amewataka wadau wa sekta za michezo, muziki na filamu Mkoani Arusha kujisajili katika vyama husika ili waweze kutambulika rasmi.

Akizungumza na wadau hao leo Mkoani Arusha , Dkt. Mwakymbe amesema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo wanamichezo na wasanii wa filamu na maigizo ni kukosa umoja na kutokujisajili hivyo kuzuka kwa migogoro.

“Tatizo kubwa linalowakabili wanamichezo na wasanii wa filamu nchini ni kutokufuata sheria , kanuni na taratibu zilizowekwa , jambo ambalo linaleta shida kuwatambua na kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yenu” amesema Dkt. Mwakyembe

Amefafanua kuwa, kujisali na kutambulika kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pamoja na Bodi ya Filamu ni muhimu katika utendaji wa kazi na endapo changamoto yeyote inajitokeza basi inakuwa rahisi kutatuliwa.

Aliwaahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini Bw. Gabriel Daqarro amewataka wadau hao kuhakikisha wanawasilisha matatizo yao kwa Afisa Michezo wa Mkoa ili yaweze kufanyiwa kazi.

“Ni muhimu kuwasiliana na Afisa Michezo na Afisa Utamaduni ili kuwasilisha changamoto zenu na wao wataziwasilisha ngazi za juu kwa ajili ya utatuzi kuliko kusubiri vikao, kwani baadhi ya changamoto ziko ndani ya uwezo wetu” amesema Bw. Daqarro.

Naye Afisa Michezo Mkoa Bi. Mwamvita Okeng’o ameahidi kushirikiana kwa karibu na wadau hao katika kuleta maendeleo ya sekta ya michezo mkoani hapo.