Dkt. Mwakyembe Awataka Washiriki wa Ulimbwende Kutokuoana Aibu Kutumia Lugha ya Kiswahili Katika Mashindano ya Dunia.


Imewekwa 09th September, 2018

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka washiriki wa mashindano ya ulimbwende nchini, kutokuona aibu kutumia lugha ya Kiswahili katika mashindano ya Urembo ya Dunia (Miss World) ili kuitangaza zaidi lugha hiyo.

Hayo ameyasema jana Jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi katika fainali za ulimbwende (Miss Tanzania) zilizofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, ambapo warembo 20 kutoka mikoa mbalimbali nchini walichuana kuwania taji hilo.

“ Tumieni lugha ya Kiswahili mnapojibu maswali hata katika mashindano ya nje, nimeona warembo wengi wanaoshiriki mashindano ya dunia wakitumia lugha za kwao wanapojibu maswali hivyo msione aibu kutumia lugha hii” alisema Dkt. Mwakyembe

Aidha Dkt. Mwakyembe anazidi kufafanua kuwa katika lugha zinaongoza kwa kuongewa duniani mojawapo ni Kiswahili ambayo ni lugha ya 10 kati ya lugha 6000 zinazosemwa kwa wingi duniani, pia ni lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika.

Vilevile amewataka washiriki hao kutumia jukwaa hilo la ulimbwende kama fursa ya kutangaza vivutio mbalimbali za asili na utalii vinavyopatikana nchini ili kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi .

“Ulimbwende ni sanaa yenye nafasi kubwa sana hasa katika kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya Utalii na Maliasili hapa nchini” alisema Dkt. Mwakyembe

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya The Look ambaye pia aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 1998 na muaandaji wa mashindano hayo Bi. Basila Mwanukuzi ameeleza kuwa washindi walioingia tano bora mbali na kushika nafasi hizo, pia watakuwa mabalozi wa kutangaza sekta ya Utaliia katika hifadhi mbalimbali.

Mashindano ya ulimbwende ya Tanzania yamefinyika kwa mara ya kwanza baada ya kusimamishwa mwaka 2016 , huku mshindi wa kwanza wa taji hilo Bi. Queen Elizabeth akiibuka na ushindi wa gari aina ya Terrious pamoja na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia yanaotarajiwa kufanyika Sanya,nchini China.