Dkt. Mwakyembe aipongeza India kwa Kutimiza miaka Sabini ya Uhuru.


Imewekwa 29th November, 2017

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe ameipongeza Jamhuri ya India kwa kutimiza miaka 70 tangu ilipopata Uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1947.

Waziri Mwakyembe ametoa pongezi hizo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za maadhimisho hayo ambapo ameipongeza nchi hiyo kwa kuendelea kuuenzi na kuulinda Utamaduni wao hata wakiwa nje ya India.

“Nawapongeza sana kwa kutimiza miaka 70 ya Uhuru ni jambo la kujivunia sana,lakini pia nawapongeza kwa kuendelea kuuenzi Utamaduni wenu kwa kila nyanja, na nawahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na nyie katika kuleta maendeleo miongoni mwetu.”Alisema Waziri Mwakyembe.

Naye Balozi wa India hapa nchini Mhe.SanDeep Arya emeishukuru Serikali kwa ushirikiano inaowapa katika maeneo mbalimbali yenye manufaa kwa mataifa hayo mawili na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo wa kidiplomasia uliopo baina yao.

“India inafarijika sana na ushirikiano huu ulipo miongoni mwetu,tunaahidi kushirikiana zaidi hasa katika Sekta ya Utamaduni ambayo Serikali imeonyesha jitihada zake katika kuendeleza na kuimarisha kwa kuwa utamaduni ndio unaotambulisha mtu popote anapokuwa.”Alisema Balozi Arya.

Katika sherehe hizo watu waJamhuri ya India walionyesha Utamaduni wao kwa kucheza ngoma mbalimbali za Taifa hilo,nyimbo, pamoja na michezo mingine ya kihindi ikiwa ni kuendeleza na kudumisha Utamaduni wa nchi hiyo.