Bodi ya Filamu fanyeni utafiti kuona takwimu za mapato ya sekta ya filamu – Mhe. Shonza


Imewekwa 27th October, 2017

Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza ameitaka Bodi ya Filamu Tanzania kufanya utafiti na kukusanya takwimu sahihi za mapato yatokanayo na sekta ya filamu nchini ili kuweza kubaini sekta hiyo inavochangia katika pato la taifa.

Hayo ameyasema jana Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania na kuzungumza na watendaji wa bodi hiyo huku akiwataka kuweka mifumo ambayo itasaidia wasanii kuinua, kuboresha na kuendeleza tasnia ya filamu nchini.

Aidha Mhe. Shonza ameitaka bodi ya filamu kuhakikisha kuwa inasimamia maadili katika filamu pamoja na ubora wa filamu ili filamu zinazotengenezwa inchini ziwe na kiwango kitakachowavutia wadau wa filamu ndani na nje ya nchi kupenda filamu zetu.

Mhe. Shonza amesema kuwa katika kukuza vipaji Bodi ya filamu ifanye jitihada za kuwafikia na kutoa elimu kwa wanatasnia ya filamu waliopo mikoani kwani huko nako kuna wasanii wenye uwezo wa hali ya juu lakini vipaji vyao havionekani kutokana na kutofikiwa kwa wakati.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amemhakikishia Mhe. Naibu Waziri kuwa Bodi ya Filamu itaendelea kukaza kamba na kuhakikisha kuwa haioni haya katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu ya sheria na kanuni zilizopo.

Bibi. Fissoo amesema kuwa kati ya mwaka 2011 hadi sasa bodi ya filamu imesambaza jumla ya nakala elfu thelathini za sheria na kanuni katika Mikoa na Wilaya zote nchini ili shughuli za filamu zinazofanywa mikoani ziweze kuendana na sheria na kanuni zilizopo katika sekta ya filamu.

Naye Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Bw. Simon Mwakifwamba amemshukuru Naibu Waziri Shonza kwa kuonyesha hari ya kuipigania sekta ya filamu mara tu baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri kwani kwa kufanya hivyo kunawapa moyo wanatasnia ya filamu kuelekea katika mapinduzi ya filamu nchini.